Mwawakilishi wa Tanzania katika shindano la Big Brother nchini Afrika Kusini, Lotus Kyamba ameondolewa ndani ya jumba hilo kwa utovu wa nidhamu baada ya kugombana na mshiriki mwenzake Luclay wa Afrika Kusini.
Tukio hilo limetokea leo mchana, wakati washiriki hao walipokuwa kwenye bustani ya jumba hilo wakiendelea na zoezi maalum walilopewa na Biggie, ambako ghafla wawili hao walianza kutupiana maneno makali yakiwamo matusi, kabla ya Lotus kupandwa na munkari na kumvamia Luclay raia wa Afrika Kusini na kumzaba kibao.
Baada ya hali hiyo, uongozi wa shindano hilo uliamua kumfukuza Lotus kwa kitendo chake hicho kilichoenda kinyume na sheria za shindano.
Awali, kabla ya Lotus hajachukua uamuzi wa kumchapa kibao hicho, Luclay alianza kamtolea maneno makali ikiwemo kumkebehi kwa kumtishia Mtanzania huyo kuwa amwache, kwani yupo katika nchi yake na hawezi kumfanya kitu, jambo lililomuongezea hasira zaidi kufikia hatua hiyo ya kumvaa.
Mzozo huo uliamuliwa na washiriki wenzao, wakiwemo Mganda, Ernest, Mkenya Nic na Methiopia Danny, ambapo walimuwahi Luclay na kumsihi kutojibu mapigo na badala yake awatii.
Kitendo cha Lotus kuondoka jumbani, washiriki wenzake walimuaga kwa mara ya mwisho huku wote walionekana kuwa na huzuni kubwa, ambako Danny, Bhoke, Nic, Nkuli, Karen pamoja na Luclay walionekana kububujikwa na machozi, kwani hawakutegemea kama ingetolewa adhabu hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Habari Mkuu wa Multchoice Tanzania, Barbara Kambogi alisema kuwa, wamesikitishwa na jambo hilo, kwani hawakutegemea hivyo na wanajipanga kuona hali itakavyokuwa, ikiwemo harakati za kumpokea atakapotua nchini.
Shindano hilo la mwaka huu limejaa kila aina ya visa, ikiwemo ubabe kwa washiriki hao ambako karibu washiriki wote wamegombana.